Ndege ya Shirika la Ndege la Ukraine iliyokuwa na watu 180 (abiria pamoja na wafanyakazi wa ndege) imeanguka muda mfupi baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Imam Khomeini jijini Tehrani, Iran mapema leo alfajiri.
Taarifa za awali kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa watu wote waliokuwemo katika ndege hiyo wamefariki dunia.
Kwa mujibu wa FligohtRadar 24 ambao hutoa taarifa kuhusu huduma za ndege imesema kuwa ndege hiyo, Boeing 737-800 jet, imeanguka kutokana na hitilafu za kiufundi imekuwa ikitoa huduma kwa miaka mitatu na nusu sasa.
Ndege hiyo ilikuwa inatarajiwa kuruka saa 11:15 alfajiri kwa saa za Tehran kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boryspil uliopo katika Mji Mkuu wa UKraine, Kiev, ilichelewa kuanza safari ambapo iliruka saa 12:12 alfajiri kwa saa za huko.
Vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vinatofautiana kuhusu idadi kamili ya watu waliokuwamo ndani ya ndege hiyo.
Msemaji wa Shirika la Usafiri wa Anga nchini Iran, Reza Jafarzadeh amesema kuwa tayari timu ya uchunguzi imepelekwa eneo la tukio na kwamba taarifa za kina kuhusu ajali hiyo zitatolewa.
Kampuni ya Boeing ambayo ndiyo mtengenezaji wa ndege hiyo imesema kuwa inafahamu kuhusu ajali hiyo, lakini bado inaendelea kukusanya taarifa zaidi.
Ajali hiyo imetokea saa chache baada ya Iran kushambulia kambi mbili za kijeshi zinazokaliwa na wanajeshi wa Marekani, ikiwa ni tukio la kulipiza kisasi kufuatia Marekani kumuua kiongozi wa Jeshi la Iran, Jeneral Qasem Soleimani.