Wenye mafua kutoruhusiwa kupanda vivuko

0
943

Serikali ya Kenya imesema kuwa itakuwa inawapima wananchi wote wanaotumia vivuko vinavyounganisha Mji wa Mombasa na Kaunti ya Kwale, na wale wote watakaoonesha dalili za mafua hawatoruhusiwa kutumia usafiri huo.

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho akitangaza utaratibu huo mpya amesema kuwa watu wote wanaotumia vivuko ni lazima wavalie barakoa, au wafunike midomo na pua zao kwa kutumia kitambaa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya watu wenye maambukizi ya virusi vya Corona kubainika kwenye maeneo hayo mawili.

Akizungumzia uamuzi huo Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Gilbert Kitiyo amesema kuwa mtu yeyote mwenye dalili za maambukizi ya virusi vya corona aepuke kutumia vivuko hivyo, badala yake aende kwenye vituo vya afya kwa ajili ya msaada zaidi.

Mbali na hatua hiyo mamlaka zimesema zitatekeleza agizo la kuhakikisha kuwa watu hawakai karibu karibu wanapotumia usafiri huo wa majini.

Jumanne (Machi 24) waziri wa afya wa Kenya alitangaza kuwa watu 25 wamethibitika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya mapafu.