Waziri wa Fedha wa Kenya, – Henry Rotich amefikishwa mahakamani jijini Nairobi, akituhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya, – Noordin Haji amesema kuwa Rotich pamoja na maafisa wengine wa serikali, wanatuhumiwa kukiuka taratibu za utoaji wa Kandarasi ya zaidi ya Dola Milioni 450 za Kimarekani iliyopewa kampuni ya Cmc Di Ravenna ya nchini Italia, kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili ya maji.
Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa, mabwawa hayo mawili ya maji yalidaiwa kujengwa katika jimbo la Elgeyo Marakwet, lakini mpaka sasa fedha za ujenzi wa mabwawa hayo hazijulikani zilipo na mabwawa hayo hayajajengwa.
Hapo jana, Rotich alijisalimisha kwa Maafisa wa upelelezi, muda mfupi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya kuagiza akamatwe.
Kampuni hiyo ya Cmc Di Ravenna pamoja na Waziri Rotich wamekanusha tuhuma hizo.