Mjini Kabul watu wenye silaha wamefanya mashambulizi mashariki mwa jimbo la Nangarhar na katika hospitali ya serikali ya ya Dashti Barchi mjini humo ambapo wamepambana na vikosi vya ulinzi katika hospitali hiyo na kusababisha hali ya taharuki kwa wagonjwa na watoa huduma.
Madaktari wasio na mipaka wanaotoa huduma katika hosipitali hiyo ya wanawake na watoto wamekuwa na kazi ngumu ya kuondoa watoto wachanga na mama baada ya jengo la hospitali hiyo kuwaka moto wakati wa mapambano kati ya watu hao wenye silaha na walinzi wa serikali.
Msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Tareq Arian amesema zaidi ya wanawake 80 na watoto wao wameokolewa na kupelekwa katika hosipitali ya karibu.
Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu 17 huku picha zikionyesha moshi mzito kutoka katika eneo la hospitali.