Wasimulia njaa, mauaji, ubakaji vita vinavyoendelea Sudan

0
184

Raia walionaswa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan wametoa maelezo kuhusu ubakaji, ghasia za kikabila na watu kunyongwa mitaani.

Waandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wamefanikiwa kufika mstari wa mbele wa mapigano hayo karibu na mji mkuu, Khartoum na kuzungumza na watu mbalimbali.

Maofisa wa Umoja wa Mataifa wamesema mzozo huo umeitumbukiza nchi hiyo katika “mojawapo ya jinamizi baya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni” na linaweza kusababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani.

Pia kuna hofu kwamba huko Darfur, magharibi mwa nchi, marudio ya kile Marekani ilichoita mauaji ya halaiki ya miaka 20 iliyopita yameanza kujitokeza.

Wanawake kadhaa wamesimulia namna ambavyo wamekuwa wakibakwa huku wengine wakisimulia namna mauaji ya kikabila yanavyoendelea nchini humo, husuani katika Jimbo la Darfur.

“Wanakuuliza wewe ni kabila gani, kama wewe ni kabila la Masalit, wanakuua,” amesemulia mmoja wa walionusirika na mauaji katika vita hivyo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya vikundi viwili hasimu vya Serikali ya Kijeshi ya Sudan (SAF) chini uongozi wa Abdel Fattah al-Burhan, na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) kinachoongozwa na aliyekuwa msaidizi wa Burhan jeshini, Jenerali Mohamed Dagalo maarufu Hemedti, vilivyoanza Aprili 15 mwaka jana, vimeshaua watu wanaokadiriwa kufikia 14,000.