Wanafunzi wa kike 279 waliotekwa nyara katika shule moja ya bweni iliyopo kwenye jimbo la Zamfara nchini Nigeria, wameachiwa huru.
Kamishna wa Ulinzi na Mambo ya Ndani wa jimbo la Zamfara, – Abubakar Muhammad Dauran amesema kuwa, kwa sasa Wanafunzi hao wamewekwa katika kituo kimoja kilichopo katika makao makuu ya jimbo hilo Gusau.
Amesema idadi iliyotolewa awali ya Wanafunzi 317 kutekwa nyara si sahihi, kwa kuwa baada ya kufanyika uhakiki wa kina wamebaini ni Wanafunzi 279 ndio waliotekwa nyara.
Amesema Wanafunzi hao wameachiwa huru baada ya kufanyika kwa majadiliano yaliyoshirikisha watekaji hao na kwamba hakuna malipo yoyote yaliyofanyika.
Wanafunzi hao wa kike walitekwa nyara Februari 26 mwaka huu na watu wenye silaha, ambao walivamia shule moja inayomilikiwa na Serikali iliyopo kwenye mji wa Jangebe katika jimbo hilo la Zamfara.