Wakili wa Bobi Wine azuiliwa kuingia Uganda

0
2401

Wakili wa kimataifa aliyepewa kazi ya kumwakilisha Mbunge wa Kyadondo Mashariki nchini Uganda, – Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amezuiwa kuingia nchini humo.

Robert Amsterdam ambaye ni raia wa Canada ameorodheshwa kama mtu asiyetakiwa na serikali ya Uganda.

Amsterdam ni miongoni mwa mawakili walioorodheshwa kumtetea Bobi Wine katika kesi yake ambapo ameshtakiwa kwa uhaini.

Jukumu la Amsterdam ambaye huendesha shughuli zake kupitia kampuni ya Amsterdam and Partners iliyo na ofisi katika miji wa Washington nchini Marekani na London nchini Uingereza limetajwa kuwa ni kufanya masuala ya kiufundi, kutoa ushauri na kusaidia katika utafiti.

Bobi Wine amekuwa akizuiliwa rumande katika gereza la Gulu akiwa pamoja na watuhumiwa wengine 33 kwa madai ya kuurushia mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arua.