Filamu ya mwisho ambayo mwigizaji wa Nigeria, Junior Pope alikuwa akiwatengenezea wafuasi wake zaidi ya milioni mbili kwenye Instagram iliashiria kifo chake mapema tu.
“Unaona hatari ambayo watu tunachukua ili kuwaburudisha?” Mwigizaji huyo mwenye umri wa miaka 42 anasikika akipaza sauti dhidi ya kelele za boti ndogo inayoendeshwa kwa mwendo wa kasi ndani ya Mto Niger.
Mara anasikika akicheka, haieleweki ni kwa furaha au woga, kisha anamwambia Nahodha apunguze mwendo.
“Punguza mwendo, mimi ni mtoto wa pekee na nina watoto watatu wa kiume (wananitegemea),” mwigizaji huyo, ambaye jina lake halisi lilikuwa John Paul Odonwodo, anasema kwa sauti ya juu akionesha mshtuko baada ya maji kuanza kuingia botini.
Siku iliyofuata nyota huyo wa Nollywood aliripotiwa kufa maji kwenye mto huo baada ya boti hiyo aliyokuwa akitumia kutengeza movie yake kugongana na mtumbwi wa uvuvi na kuzama.
Watu wengine wanne, wakiwemo waliokuwa wakishiriki kuzalisha filamu yake pia walipoteza maisha.
Kifo cha staa huyo kilichojiri mwezi Aprili kimetikisa tasnia ya filamu nchini Nigeria na sasa wasanii na hata serikali imeshtuka.
Ripoti ya awali kutoka Ofisi ya Uchunguzi wa Usalama ya Nigeria imeonesha mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na nahodha wa boti hakuwa ameidhinishwa na mamlaka husika na hata boti yenyewe haikuwa imesajiliwa.
Mtu mmoja tu alikuwa amevaa jaketi la tahadhari na ni miongoni mwa watu wanane walionusurika!
Nigeria (Nollywood ) ni nchi ya tatu duniani kwa kuzalisha filamu baada ya Hollywood (Marekani) na Bollywood (India). Inazalisha zaidi ya filamu 2,500 kwa mwaka na kutengeneza ajira lukuki.
Chanzo: BBC