Ethiopia imewaachia huru Wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la nchi hiyo baada ya Wafanyakazi hao kukiuka taratibu za kuingia katika jimbo la Tigray.
Msemaji wa Serikali ya Ethiopia, – Ridhiwan Hussein amesema Wafanyakazi hao wa Umoja wa Mataifa waliokuwa katika magari yaliyobeba shehena ya misaada, walikamatwa baada ya kuvuka vizuizi viwili katika barabara inayoelekea jimbo la Tigray bila kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali ya Ethiopia.
Amesema Wanajeshi wa Ethiopia walitoa ishara mbalimbali za kuwazuia bila mafanikio ambapo walilazimika kufyatua risasi ili kuzuia msafara wa Wafanyakazi hao ambao amesema walikuwa wamekaribia kizuizi cha tatu katika barabara hiyo.
Hata hivyo msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema Wafanyakazi hao walikuwa na zoezi la ukaguzi wa barabara hiyo ambayo amedai ni miongoni mwa zile zitakazotumika kufikisha misaada mbalimbali ya kibinadamu katika jimbo la Tigray lenye mgogoro huko nchini Ethiopia.