Wafanyakazi wa afya kuanza kutoa huduma

0
1175

Wafanyakazi wa afya ambao wamekua wakiwasaidia wagonjwa wa Ebola katika mji wa Beni uliopo kwenye Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameanza tena kutoa  huduma,  baada ya kusitisha kwa muda wa siku mbili kufuatia shambulio la waasi lililosababisha vifo vya watu 18.

Wafanyakazi hao wameanza kutoa huduma hizo za afya kufuatia onyo lililotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa kuendelea kusitishwa kwa huduma hizo kunaweza kusababisha madhara zaidi.

Katika taarifa yake, WHO  imesema kuwa jitihada za kukabiliana na Ebola ni lazima ziendelee kwa kuwa kwa kutofanya hivyo kunaweza kusababisha kuenea kwa ugonjwa huo hadi katika eneo la mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Uganda.

Kwa sasa Wafanyakazi hao wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wataendelea kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Ebola na kutafuta watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa huo ili waweze kupatiwa matibabu.