Waathirika wa Idai waendelea kupata msaada

0
563

Meli iliyobeba msaada wa tani Elfu Mbili za chakula, maji na dawa  uliotolewa na raia wa kawaida wa Msumbiji kwa ajili ya kuwasaidia wenzao walioathiriwa na kimbunga Idai siku 12 zilizopita, imewasili katika mji wa Beira.

Kazi inayoendelea sasa baada ya kuwasili kwa msaada huo, ni kuusambaza kwa watu mbalimbali walioathiriwa na kimbunga hicho.

Mbali na kazi ya kusambaza msaada huo wa chakula, maji na dawa, wafanyakazi wa Idara ya Ujenzi nchini Msumbiji wanaendelea na matengenezo ya barabara zilizoharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai.

Nalo Shirika la Msalaba Mwekundu limesema kuwa limepokea ombi la kuipatia Msumbiji msaada wa dharula wenye thamani ya zaidi ya Dola Milioni Thelathini za Kimarekani , utakaotumiwa na watu walioathiriwa na Kimbunga Idai.

Zaidi ya watu 700 wamethibitika kufa hadi hivi sasa,  kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Idai katika nchi za Msumbiji, Zimbabwe  na Malawi na habari zaidi zinasema kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.