Nchi ya Burundi imewataka waangalizi wa uchaguzi mkuu wanaotarajiwa kuingia nchini humo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kukumbuka kwamba watakaa katika uangalizi maamlum kwa siku 14 kufuatia uwepo wa maambukizi ya virusi vya CORONA.
Mpaka sasa zimebaki siku nane kufanyika kwa uchaguzi huo hivyo wale ambao bado hawajafika nchini humo au wale ambao hawakuweza kufika nchini humo siku 13 zilizopita hawataweza kupata nafasi ya kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Serikali ya Burundi na kutiwa saini Mei 8, kila mtu anayeingia nchini humo awe mgeni au raia lazima atii awekwe chini ya uangalizi maalum.
Barua hiyo imetoa ushauri kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwatumia wajumbe ambao tayari wako nchini humo muda mrefu kufanya kazi hiyo na wasio wafanyakazi wa jumuiya hiyo nchini humo.
Tume huru ya uchaguzi nchini Burundi mpaka sasa haijatangaza orodha ya mwisho ya wagombea na kuna uwezekano majina yakatoka siku ya mwisho.