Virusi vya Corona vyasadikika kuingia Kenya

0
524

Mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona amewekwa katika uangalizi maalum katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta (KNH) jijini Nairobi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Taarifa ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) imeeleza kuwa abiria huyo amewasili jijini Nairobi leo Januari 28, akitokea Guangzhou nchini China ambapo ndipo virusi hivyo vilipoenea kwa kiwango kikubwa.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa uamuzi wa kumuweka abiria huyo chini ya uangalizi maalumu umefikiwa na serikali kupitia kitengo cha afya kilichowekwa uwanjani hapo.

Ripoti inaonesha kuwa abiria huyo aliruhusiwa na mamlaka za afya mjini Guanzhou kurejea Kenya lakini alipofika ameonesha kuwa na dalili zinazoshabihiana na ugonjwa huo. KQ imesema ilichukua hatua za tahadhari kwa kumtenga abiria huyo wakati wote wa safari.

Hadi sasa watu zaidi ya 100 wameripotiwa kufariki dunia kutokana na virusi hivyo nchini China, huku vikizidi kusambaa kwenda katika maeneo mbalimbali duniani.