Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amesema suala la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19) bado ni tatizo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo bado jitihada madhubuti zinafanyika katika kupambana na ugonjwa huo.
Akizungumza katika Mkutano wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaofanyika nchini Malawi, Rais Chakwera ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo amesema nchi za SADC tayari zimeingia kwenye mpango wa chanjo ya UVIKO 19 (COVAX).
Awali, Katibu Mtendaji wa SADC anayemaliza muda wake, Dkt. Stagomena Tax ameishauri jumuiya hiyo kushughulikia changamoto zinazoikabili ukanda huo kama umaskini, ugaidi, tatizo la ajira na uhalifu wa mitandao.
Katika hotuba yake Dkt. Tax amesema moja ya mafanikio anayojivunia katika uongozi wake ni Kiswahili kutumika kama lugha ya mawasiliano katika jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 16.
Kutokana na changangomoto za UVIKO 19 baadhi ya washiriki wameshindwa kuhudhuria ambapo Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Moussa Mahamat na mwakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Vera Songwe wametoa hotuba zao kwa njia ya video.
Katika Mkutano huo wa 41 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, Jamhuri ya Malawi itathibitishwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja (Agosti 2021 – Agosti 2022).