Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limewataka viongozi wa Ethiopia wafungue njia kuliwezesha shirika hilo kuzifikia kambi za wakimbizi wa Eritrea zilizoko katika eneo la Tigray.
Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch amewaeleza waandishi wa habari kwamba wana wasiwasi mkubwa kutokana na ripoti zinazowafikia za kufanyika mashambulio na mapigano karibu kabisa na kambi hizo.
Amesema, “tunasikia habari za utekaji nyara watu na kuhamishwa kwa nguvu, kwa hiyo ni muhimu sana kwetu kupatiwa ruhusa ya kufika kwenye kambi hizi ili tuweze kuona ni nini hasa kilichotokea huko.”
Katika kambi hizo kuna wakimbizi 96,000 ambao akiba ya chakula chao imemalizika tangu mwezi uliopita.
Eneo la Trigray lililoko Kaskazini mwa Ethiopia katika wiki za karibuni limekuwa uwanja wa vita na mapigano kati ya jeshi la serikali kuu na wapiganaji wa harakati ya ukombozi ya watu wa Tigray (TPLF).
Serikali ya Addis Ababa ambayo inalituhumu eneo la Tigray kuwa linataka kujitenga, hivi karibuni imetangaza kuwa vikosi vya jeshi vimeushikilia kikamilifu mji mkuu wa eneo hilo Mekelle.
Habari kutoka eneo la Tigray zinaeleza kuwa unyongaji holela wa watu na mauaji ya mamia ya raia yamefanyika wakati wa vita na mapigano kati ya jeshi la serikali na vikosi vya TPLF..