Unafahamu nini kuhusu Jumamosi Kuu?

0
483

Jumamosi Kuu au kwa majina mengine Jumamosi Takatifu, kwa waumini wa dini ya Kikristo ni siku moja kabla ya Jumapili ya Pasaka ambayo ni siku ya mwisho ya Wiki Takatifu.

Siku hii ni siku muhimu katika kalenda ya kiliturujia ya madhehebu mengi ya Kikristo, ikiwa ni pamoja na Kanisa Katoliki, Kanisa la Orthodox la Mashariki na Usharika wa Anglikana, Lutheran na madhehebu mengine ambayo wanaamini juu ya ufufuo wa Yesu Kristo.

Makanisa mengi huwa na ibada maalumu siku hii ikiwa ni pamoja na Mkesha wa Pasaka ambao ni ibada ya kusherehekea kufufuka kwa Yesu Kristo.

Kwa kawaida mkesha wa Pasaka kwa baadhi ya makanisa huanza baada ya jua kuzama siku ya Jumamosi Takatifu huku ikijumuisha kuwasha mshumaa wa Pasaka, kusoma maandiko na kusherekea Ekaristi.

Wakristo wengine huadhimisha siku hii kwa maombolezo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ambayo mwili wa Yesu Kristo ulihifadhiwa kaburini baada ya kusulubishwa, na kungojea ufufuo wake.
Kwa upande mwingine waumini wa dini ya Kikristo huitumia siku hii kukumbuka dhabihu ambayo Yesu Kristo aliitoa kwa ajili ya dhambi zao na kutafakari maana ya kifo na ufufuo wake.

Kulingana na tamaduni na imani ya dini ya Kikristo, Jumamosi Takatifu ni siku ya kufunga na kujizuia, ni sikukuu na makanisa mengi hufanya ibada zenye maudhui ya kutafakari kwa utulivu.

Kwa makanisa mengine hubadilisha mtindo wa upambaji katika madhabahu zake na huacha giza katika kanisa kama ishara ya kutokuwepo kwa Yesu Kristo.

Hata hivyo, siku hii ni siku ya matumaini na ni siku ya mwisho kwa kipindi cha mfungo na toba ‘Kwaresma’. Ni wakati wa kutazamia furaha ya Jumapili ya Pasaka ambapo Wakristo huamini ndio siku alipofufuka Yesu Kristo.