Umoja wa Afrika yajiandaa kusuluhisho mgogoro nchini Congo

0
925


Umoja wa Afrika Au umetoa wito wa kusuluhisha kwa amani mzozo wowote utakaotokana na matokeo ya uchaguzi nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo yaliyompatia ushindi mgombea wa upinzani Felix tshisekedi .

Taarifa kutoka ofisi ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat imesema ni muhimu kwamba tofauti zozote kuhusu matokeo hayo yaliotangazwa na Tume ya uchaguzi  yatafutiwe muafaka wa kitaifa kwa kuheshimu kanuni za demokrasia pamoja na kulinda na kuimarisha amani.

Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limesisitiza kuwa  matokeo ya awali hayawiani na takwimu zilizokusanywa na wasimamizi wake.

Mapema hapo jana Kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi alitangazwa kuwa mshindi wa uraisi  nchini humo lakini mgombea mwenzake wa upinzani Martin  Fayulu ameyapinga matokeo hayo kwa kusema  ni ya udanganyifu.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic amesema kwa sasa wanasubiri ufafanuzi kutoka kwa waangalizi wa Kimataifa huku ikizitaka pande zote kujiepusha na vurugu na kuonya kuwa matokeo ya mwisho yanapaswa kuendana na matakwa ya raia wa Congo.