Umoja wa Afrika wataka kusitishwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi Congo

0
1218

Umoja wa Afrika AU umeomba kusitishwa kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais ambayo yanaendelea kuibua maswali mengi nje na ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais wa Umoja huo Paul kagame amekutana na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (Icglr) katika mkutano wa faragha ulodumu takriban saa tano.

Katika taarifa yao ya mwisho ya mkutano huo wameomba mamlaka nchini Drc kusitisha mpango wa kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais baada ya kubaini kuna mashaka makubwa katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais na ule wa wabunge na magavana wa mikoa yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (Ceni).

Viongozi hao wamesema wanatarajia kutuma  ujumbe wa ngazi ya juu mjini Kinshasa kukutana na mamlaka husika.

Ujumbe huo utaundwa na rais wa sasa Umoja wa Afrika Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, na viongozi wengine ambao walihudhuria mkutano huo.

Mahakama ya Katiba inatarajia kutangaza baadae leo matokeo ya mwisho ya uchaguzi wa urais wa Desemba 30, 2019.