Uganda kutumia trilioni 47.2 mwaka 2022/2023

0
178

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema serikali ya nchi hiyo itaendelea kuongeza fedha katika bajeti kila mwaka ili kuwezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ikiwemo ya maendeleo na huduma za kijamii.
 
Akizungumza katika viwanja vya Kololo jijini Kampala ambavyo vimetumika kama ukumbi wa bunge kwa ajili ya usomwaji wa bajeti hii leo, Rais Museveni amesema sehemu kubwa ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 inayofikia shilingi trilioni 47.2 ni fedha za ndani.
 
Akitangaza bajeti hiyo Waziri wa Fedha na Mipango wa Uganda, Amos Lugoloobi amesema vipaumbele vimewekwa katika kuboresha sekta ya kilimo cha kibiashara, kukuza viwanda pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, nishati, afya na elimu.
 
Amesema bejeti hiyo pia imelenga kuimarisha amani na usalama, kupambana na vitendo vya rushwa, kutengeneza ajira mpya, kuimarisha bei za mazao, kudhibiti mfumuko wa bei hasa zile za bidhaa ikiwemo mafuta ya kuendeshea mitambo na vyombo vya moto.