Uchunguzi wafanyika kubaini kilichompata Kashoggi

0
1954

Wachunguzi kutoka nchini Uturuki walioingia katika makazi mawili ya maafisa ubalozi wa Saudi Arabia kuchunguza matukio wanayoweza kubaini kilichomtokea mwandishi wa habari wa nchi hiyo Jamal Kashoggi wamemaliza kazi yao.

Wachunguzi hao wamesema kuwa wamepata sampuli mbalimbali zitakazowasaidia kufanya kazi waliyokuwa wametumwa kufanya kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia.

Wameongeza kuwa gari lililokuwa ndani ya ubalozi huo mdogo katika kipindi ambacho Kashoggi aliingia kwenye ubalozi huo na baadaye kuendeshwa katika makazi ya kiongozi mkuu wa ubalozi, linaweza kusaidia kutoa picha kamili ya kile kilichokuwa kikiendelea siku ya tukio.

Wachunguzi hao walilazimika kuchelewa kufanya uchunguzi wao kwa karibu saa 24 katika makazi hayo baada ya kukamilisha uchunguzi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul kwa kuwa walikosa ushirikiano kutoka kwa maafisa hao wa ubalozi.

Wakati huohuo, wabunge kutoka chama cha Democrat nchini Marekani wanamshinikiza Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuchukua hatua dhidi ya Saudi Arabia baada ya Kashoggi kupotea.

Naye Rais wa Bunge la Umoja wa nchi za Ulaya, – Antonia Tajan amesema kuwa anafuatilia kwa karibu tukio la kutoweka katika mazingira ya kutatanisha la mwandishi huyo wa habari wa Saudi Arabia,- Jamal Kashoggi.

Antonia amesema kuwa yeye mwenyewe akiwa kama mwandishi wa habari wa zamani, anafurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na watu hao na jinsi wanavyotoa muhanga maisha yao kwa ajili ya ustawi wa jamii wanayoitumikia.

Ametaka kufanyika kwa jitihada zaidi ili hatma ya Kashoggi iweze kufahamika.