Ubalozi wa Uingereza- TZ watoa neno msiba wa Malkia

0
602

Balozi wa Uingereza nchini David Concar amesema, nchi za Jumuiya ya Madola na dunia kwa ujumla zimepata pigo kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II.

Balozi Concar ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), yaliyofanyika katika makazi yake mkoani Dar es Salaam.

Amesema hatua ya raia wa nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania kuonesha kuguswa na msiba wa Malkia, ni ushahidi tosha kuwa alikuwa na umuhimu wa kipekee.

Balozi Concar amesema uhusiano uliokuwepo kati ya Uingereza na nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ikiwemo Tanzania ni wa dhati, na ni kutokana na mchango wa Malkia Elizabeth II.

Kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II, Balozi huyo wa Uingereza nchini amesema, nchi hiyo huenda ikafanya mabadiliko kadhaa.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni katika wimbo wa Taifa ambao ulikuwa ukimtaja Malkia lakini kwa sasa utamtaja Mfalme kutokana Mfalme Charles III kuwa mtawala mpya.

Mabadiliko mengine ni katika alama za kwenye fedha ambapo zilikuwa na picha ya Malkia lakini kwa sasa itabidi zioneshe picha ya Mfalme.

Balozi huyo wa Uingereza nchini David Concar ameongeza kuwa, kwa siku ya kesho huko nchini Uingereza kutakuwa na Baraza maalum la kumtambulisha rasmi Mfalme Charles III kama mtawala mpya.

Baraza hilo linaundwa na nchi ambazo zilikuwa makoloni ya Uingereza.

Kwa mujibu wa Balozi Concar, pindi zitakapopatikana taarifa rasmi za lini mazishi ya Malkia Elizabeth II yanafanyika, Ubalozi wa Uingereza nchini utaandaa ibada maalum ya kumuombea kiongozi huyo, na ni kwa ajili ya raia wa nchi hiyo waishio Tanzania.