Tshisekedi aendelea kutambuliwa

0
916

Nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Jumuiya za Kimataifa zimeendelea kumtambua Felix Tshisekedi kuwa ndiye rais ajaye wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo baada ya mahakama ya katiba ya Jamhuri hiyo  kuidhinisha ushindi wake.

Mahakama hiyo ya katiba imefikia uamuzi huo na kutupilia mbali madai ya mpinzani mkuu wa Tshisekedi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 30 mwaka 2018  Martin Fayulu,  aliyesema kuwa ndiye mshindi.

Miongoni mwa nchi za Afrika zilizotangaza kumtambua Tshisekedi ni Kenya na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambao kwa pamoja wamempongeza Tshisekedi kwa ushindi huo  na kutoa wito wa kufanyika kwa  makabidhiano ya amani ya madaraka.

Disemba 30 mwaka 2018, Fayulu aliwasilisha ombi katika mahakama hiyo ya katiba akidai kuwa kulikua na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu wakati wa uchaguzi huo na kwamba Tshisekedi amefanya makubaliano ya kugawana mamlaka na Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila, madai yaliyokanushwa na Rais huyo mteule.

Fayulu ambaye alishika nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi huo wa rais,  ameendelea kupinga matokeo hayo na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kutomtambua Tshisekedi na ameitisha maandamano ya nchi nzima kwa lengo la kupinga matokeo hayo.

Rais huyo mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwenye umri wa miaka 55, ataapishwa Jumanne Januari 22 mwaka huu ili kushika rasmi wadhifa huo wa urais.