Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa hakuna ulazima wa kuweka karantini ya kujikinga na virusi vya Corona mjini New York na New Jersey badala yake ameelekeza kuwa taarifa za ushauri ziendelee kutolewa kwa wanaotaka kusafiri ili kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo.
Trump amesema amefikia uamuzi huo baada ya mashauriano na watendaji wake na kusema amekiagiza kituo cha udhibiti na kuzuia magonjwa , CDC , kutoa ushauri kwa wasafiri utakaotekelezwa na magavana, kwa kushauriani na serikali kuu.
Suala la karantini lilipendekezwa na magavana akiwemo gavana wa chama cha Republican Ron Desantis wa jimbo la Florida, ambae alitaka kuzuia wasafiri kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi kwenda katika majimbo yao, Lakini hatua hiyo imepingwa vikali na viongozi wa majimbo hayo yanayotajwa kuwa na maambukizi makubwa, ambao wamesema hali hiyo italeta taharuki kubwa kwa wananchi.
Hadi sasa idadi ya vifo imeongezeka nchini humo na kufikia zaidi ya elfu mbili huku idadi ya walioambukizwa ikifikia 122,000