Trump anaweza kugombea urais baada ya kutiwa hatiani?

0
304

Donald Trump amekuwa Rais wa kwanza wa zamani wa Marekani kuhukumiwa kwa mashtaka ya jinai, baada ya jopo maalumu la mahakama Mjini New York kumpata na hatia katika mashtaka yote 34 dhidi yake.

Mashtaka hayo yote yanahusiana na kughushi rekodi za biashara yake ili kuficha malipo aliyolipwa nyota wa zamani wa filamu za ngono, Stormy Daniels ili kumshurutisha kutosema lolote kabla ya uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2016. Sasa ni nini kitafuata baada ya uamuzi huu?

BADO ANAWEZA KUGOMBEA URAIS?

Ndiyo. Katiba ya Marekani inaweka masharti machache ya mtu kustahiki kugombea urais: lazima awe na angalau na miaka 35, awe raia wa Marekani “mzaliwa wa asili” na ameishi Marekani kwa angalau miaka 14. Hakuna sheria zinazozuia wagombea walio na rekodi za uhalifu au kupatikana na hatia.

Lakini uamuzi huu wa hatia bado unaweza kuathiri uchaguzi wa urais utakaofanyika Novemba mwaka huu. Kura ya maoni kutoka kwa Bloomberg na Morning Consult mapema mwaka huu ilionesha kuwa asilimia 53 ya wapiga kura katika majimbo muhimu yanayoweza kuamua mshindi wa urais wa Marekani wangekataa kumpigia kura mgombea wa Republican ikiwa atapatikana na hatia.

Kura nyingine ya maoni, kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac mwezi huu, ilionesha asilimia 6 ya wapiga kura wa Trump wangekuwa na uwezekano mdogo wa kumpigia kura – hatua ambayo itaathiri matokeo katika kinyang’anyiro cha urais.

TRUMP ATAFANYA NINI SASA?

Trump amekuwa huru kwa dhamana wakati wote wa kesi na hili halikubadilika baada ya hukumu kusomwa jana.

Atarejea kortini Julai 11, 2024, tarehe ambayo Hakimu Juan Merchan amepanga kusoma hukumu baada ya hatua ya kwanza ya kumtia hatiani kumalizika.

Jaji atakuwa na mambo kadhaa ya kuzingatia katika hukumu, ikiwa ni pamoja na umri wa Trump.

Hukumu hiyo inaweza kuhusisha faini, kupewa muda wa kuangaliwa au usimamizi, au pengine kifungo.

Lakini Trump, kama marais wote wa zamani, ana haki ya kikatiba ya kulindwa maisha yote na makachero wa idara ya Secret Service.

Hii ina maana kwamba, endapo akifungwa, baadhi ya makachero watahitajika kumlinda ndani ya gereza.

Hata hivyo, itakuwa vigumu sana kuendesha mfumo wa magereza na Rais wa zamani kama mfungwa. Itakuwa hatari kwa usalama na gharama kubwa kumweka salama.