Tanzania yapendekeza mkakati wa pamoja kupambana na Ugaidi- AU

0
162

Serikali ya Tanzania imezishauri nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuwa na mpango mkakati wa pamoja katika kupambana na masuala ya ugaidi na majanga ya kibinadamu.

Akitoa pendekezo la Tanzania katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliomalizika jana usiku Jijini Malabo, Equatorial Guinea, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ambaye alimwakilishwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inapendekeza Umoja wa Afrika uwe na mpango mkakati utakaosaidia kuhakikisha kuwa nchi wanachama wanakwenda pamoja lakini pia kusaidiwa kujengewa uwezo wa kupambana na vitendo vya kigaidi.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkutano huo pia umetoa tamko la pamoja la kuimarisha utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyopitishwa miaka mingi pamoja na kuhakikisha Baraza la Amani na Usalama linakuwa na mpango maalum wa kufuatilia nyendo za kigaidi na kuzitokomeza.

Akielezea kuhusu Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania imeziomba nchi wanachama kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa pamoja wa utoaji wa huduma za kibinadamu ikiwemo tahadhari za mapema ambazo zinahitaji kupitiwa upya, kuendelezwa na kuimarishwa kwa ajili ya kupata utabiri na tafsiri sahihi ya majanga yatakayotokea na kuyafanyia kazi ipasavyo.

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuwa na ushirikiano na utekelezaji wa pamoja katika utoaji wa huduma za kibinadamu hasa jukumu la kuhifadhi wahamiaji na wakimbizi.

Aidha, mkutano wa 15 na 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliridhia kuzizuia nchi nne ambazo kushiriki mikutano ya Umoja wa Afrika kutokana na Mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia misingi ya Katiba ikiwemo mapinduzi ya kijeshi na nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Guinea na Sudan.

Kwa upande wake, Rais wa Cameroon na Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama, Paul Biya amezitaka nchi wanchama wa Umoja wa Afrika kushughulikia masuala ya kigaidi kwa umoja na mshikamano kwani bila kufanya hivyo mambo hayo hujenga na kuchochea itikadi kali hasa miongoni mwa vijana ambao ni idadi kubwa ya watu katika Bara la Afrika.

Wakuu wa Nchi na serikali katika Mkutano wa 16 wa Dharura waliridhia kwa pamoja kuwa kila mwaka tarehe 31 Januari kuwa siku ya Amani na maridhiano Barani Afrika na Rais wa Angola Mhe. João Lourenço atakuwa kinara ‘champion’ wa masuala ya amani.