Tanzania na Indonesia zafungua ukurasa mpya wa ushirikiano

0
500

Tanzania na Indonesia zimefikia makubaliano ya kujenga uwezo na ujuzi katika maeneo matano muhimu ambayo yanakwenda kufungua sura mpya ya ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Indonesia, Rais Samia Suluhu Hassan ametaja maeneo waliyokubaliana kuwa ni pamoja na mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kutumia teknolojia na zana za kisasa.

Aidha, maeneo mengine ni ushirikishwaji wa sekta binafsi katika maendeleo makubwa ya miundombinu nchini Tanzania, uendeshaji wenye tija na ufanisi kwa mashirikia ya kibiashara yanayomilikiwa na serikali, kufanya uchumi wa mataifa hayo kuwa wa kidijitali na kuendeleza na kuongeza uwezo wa rasilimali watu.

“Chini ya makubaliano haya, nchi zetu zitakuwa na sura mpya ya ushirikiano wa kina na mpana zaidi kwa manufaa ya pande zote mbili,”amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais wa Indonesia, Joko Widodo amesemea nchini yake itatekeleza yale yote waliyokubaliana na kusisitiza kwamba ni muhimu kwa mataifa hayo kuweka mifumo ya kishera itakayolinda wawekezaji.

Aidha, amemwalika Rais Samia Suluhu Hassan kutembelea Indonesia katika muktadha wa kukuza ushirikiano.

Awali, viongozi hao walishuhudia utiaji saini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo saba ikiwa ni mkakati wa kukuza ushirikiano wa mataifa hayo ulioanza tangu wakati wa harakati wa ukombozi wa bara la Afrika kutoka chini ya utawala wa kikoloni.

Maeneo ambayo mataifa hayo yamekubaliana kushirikiana kwa manufaa ya pamoja ni uchumi wa buluu, ushirikiano wa kimataifa, uhamiaji, biashara, afya, nishati na madini