Tanzania kuendelea kushirikiana na Cuba

0
256

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Salvado Valdés Mesa, mazungumzo yaliyofanyika katika mji wa Baku nchini Azerbaijan.

Wakati wa mazungumzo hayo Dkt. Mpango amesema Tanzania na Cuba zimeendelea kuwa na uhusiano thabiti katika sekta mbalimbali za maendeleo kama vile afya, elimu, viwanda na Biashara.

Ameishukuru Cuba kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa mafunzo hasa kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani ya udaktari na michezo pamoja na wataalamu kutoka nchi hiyo kufanya kazi katika hospitali mbalimbali Tanzania.

Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri baina ya mataifa hayo mawili ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Fidel Castro wa Cuba, uhusiano uliosaidia katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika wakati wa kupigani uhuru.

Kwa upande wake Makamu huyo wa Rais wa Cuba, Salvado Valdés Mesa amesema uhusiano uliopo wa muda mrefu baina ya Tanzania na nchi hiyo unathibitisha urafiki, umoja na ushirikiano wa kihistoria uliodumu katika mataifa hayo.

Ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Cuba katika masuala mbalimbali katika Jumuiya za kimataifa pamoja na nia yake ya dhati ya kuendelea kushirikiana na nchi hiyo.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Azerbaijan kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote unaotarajiwa kufanyika Machi 02, 2023.