Taliban yafungia wasichana kwenda chuo

0
207

Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imesitisha mara moja elimu ya chuo kikuu kwa wasichana wote nchini humo kufuatia uamuzi wa kikao cha baraza la mawaziri la Afghanistan.

“Nyote mnaarifiwa kutekeleza mara moja agizo lililotajwa la kusimamisha elimu ya watoto wa kike hadi ilani nyingine,” ilisema barua iliyotolewa kwa vyuo vikuu vyote vya serikali na vya kibinafsi, iliyotiwa saini na Waziri wa Elimu ya Juu, Neda Nadeem.

Hatua hiyo imeibua taharuki kimataifa huku Marekani ikilaani vikali uamuzi huo na kusema “Taliban haiwezi kutarajia kuwa mwanachama halali wa jumuiya ya kimataifa hadi waheshimu haki za wote nchini Afghanistan. Uamuzi huu utakuja na madhara kwa Taliban,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kuwa Guterres hajapendezwa na agizo hilo. “Katibu mkuu anakariri kwamba kunyimwa elimu sio tu kwamba kunakiuka haki sawa za wanawake na wasichana, lakini kutakuwa na madhara makubwa katika mustakabali wa nchi,” Stephane Dujarric alisema katika taarifa yake.

Marufuku ya elimu ya juu inakuja chini ya miezi mitatu baada ya maelfu ya wasichana na wanawake kufanya mitihani ya kujiunga na chuo kikuu kote nchini, huku wengi wakitamani kuchagua ualimu na udaktari kama taaluma ya baadaye.