Taasisi Afrika zatakiwa kuanzisha hifadhi binafsi za chakula

0
363

Taasisi zisizo za Kiserikali Barani Afrika zimeshauriwa kutafuta fedha kutoka kwa wahisani na watu wenye uwezo barani humo kwa ajili ya kuanzisha hifadhi binafsi za chakula ili kuzisaidia familia zinazoishi kwenye mazingira magumu.

Hayo yamebainishwa katika jimbo la Tennesee nchini Marekani na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi binafsi ya hifadhi ya chakula ya Mid South Bank, Cathy Pope baada ya ujumbe wa Waandishi wa habari 14 kutoka Afrika kutembelea hifadhi hiyo iliyopo katika jiji la Memphis lililopo katika jimbo la Tennesee.

Amesema taasisi hiyo hupata msaada wa chakula na fedha kupitia wahisani mbalimbali likiwemo Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), na chakula hicho hutolewa kwa walengwa ambao wengi ni familia zenye watu wenye ulemavu na familia zenye vipato vidogo visivyotosheleza.

Baadhi ya familia zisizo na uwezo zinazonufaika na mpango huo zimesema mpango huo unawasaidia hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi umetetereka duniani kutokana na janga la UVIKO -19 na mabadiliko ya Tabianchi ambayo yamesababisha bei ya chakula kuongezeka.

Hifadhi ya chakula ya Mid South ina uwezo wa kuhifadhi takribani tani Milioni 5 za chakula na kusambaza takribani tani Milioni 2.5 za chakula kwa mwezi ambazo hutolewa bure kwenye familia zenye mahitaji ya chakula katika miji 31 ndani ya jimbo la Tennesee.