Sunak njia nyeupe Uwaziri Mkuu Uingereza

0
445

Aliyewahi kuwa waziri wa Fedha wa Uingereza Rishi Sunak, anatarajiwa
kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo baada ya mgombea mwenzake Penny Mordaunt kujiondoa katika mchakato huo.

Mordaunt amejiondoa katika mchakato huo dakika chache kabla ya kumalizika kwa muda wa kuomba kuungwa mkono na wabunge wa chama chake cha Conservative.

Sunak atamrithi Liz Truss ambaye takribani wiki saba zilizopita walikuwa wote katika kinyang’anyiro kama hicho cha kuwania wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Ili kupata ridhaa ya kuwa waziri Mkuu wa Uingereza, mgombea anahitaji kuungwa mkono na wabunge wasiopungua mia moja na Sunak tayari aliungwa mkono na wabunge zaidi ya 190.

Rishi Sunak mwenye umri wa miaka 42 anakuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Uingereza mwenye asili ya Asia na Waziri Mkuu mwenye umri mdogo nchini humo.

Mchakato wa kupata Waziri Mkuu mpya wa Uingereza unafanyika zikiwa zimepita siku chache baada ya kujiuzulu kwa Liz Truss aliyehudumu katika nafasi hiyo kwa siku 45.