Sudan Kuwashitaki Maofisa Nane wa Jeshi la Nchi Hiyo

0
291

Serikali nchini Sudan imesema itawafungulia mashitaka maofisa wakuu wanane wa jeshi la nchi hiyo kwa madai ya kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadam na kusababisha vifo vya raia nchini humo.

Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa, hatua ya kufunguliwa mashtaka kwa maofisa hao wa jeshi, inatokana na majibu ya  uchunguzi uliofanyika kubaini chanzo cha mauaji ya raia takribani mia moja na thelathini wa Sudan wakati jeshi la nchi hiyo lilipotumia nguvu kuwatawanya waandamaji waliokusanyika nje ya makao makuu ya jeshi, June Tatu Mwaka Huu.

Akizungumzia hatua hiyo, kiongozi wa tume iliyofanya uchunguzi huo, Fath Al- Rahman Said, ambaye hakuwataja kwa majina maofisa hao wa jeshi, amesema Maofisa watatu kati ya hao wanane, waliruhusu matumizi ya nguvu ya ziada kuwatanya waandamanji hao na kusababisha vifo kadhaa.

Hata hivyo vyama vya siasa na asasi za kiraia nchini humo zimepinga matokeo ya uchunguzi wa kamati hiyo na kutaka kufanyika kuwa uchunguzi mwingine huru wa madai ya ukiukwaji wa haki za binaadam na mauaji ya waandamaji nchini humo.