Sina kinyongo na waliokuwa kinyume nami

0
155

Rais Mteule wa Kenya, William Ruto amesema katika uongozi wake hatambagua yeyote na hatakuwa na kinyongo na walio kinyume naye.

Ruto ametoa kauli hiyo katika ukumbi wa Bomas, Nairobi mara baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 9 mwezi huu nchini Kenya.

Amewataka wananchi wote wa Kenya kushirikiana na kwamba wasiangalie mambo ya nyuma bali wasonge mbele.

Ruto amewashukuru wananchi wote wa Kenya waliompigia kura na hata ambao hawakumpigia kuwa kwa kumuamini na kumchagua awaongoze.

Amesema wananchi wengi wa Kenya wamekuwa pamoja naye kwa kila hali wakati wa kampeni, upigaji kura na hata kusubiri kutangazwa kwa matokeo ya Urais.

Rais huyo Mteule wa Kenya pia ameipongeza Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kwa kufanya kazi nzuri hadi kukamilisha uchaguzi huo.

Amesema tume hiyo chini ya Mwenyekiti wake Wafula Chebukati ndio shujaa wa uchaguzi huo.