Shamin Khan atunukiwa Tuzo ya juu ya heshima

0
1432

Aliyewahi kuwa Naibu Waziri kwenye wizara mbalimbali nchini, -Shamim Khan ametunukiwa tuzo ya juu ya heshima (Pravasi Bharati yan Samman Award) na Rais wa India, -Ram Nath Kovind.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kuwa, tuzo hiyo imetolewa wakati wa mkutano wa 15 wa Diaspora wa India  uliofanyika kwenye mji wa Varanasi uliopo katika jimbo la Uttar Pradesh  nchini India Januari 23 mwaka huu.

Shamim Khan ametunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii hususani katika masuala ya akina mama, pamoja na kudumisha amani na uhusiano mzuri wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini Tanzania. 

Akizungumza wakati akimtunuku tuzo hiyo, Rais Kovind  wa India amesema kuwa Shamim Khan pia amefanya kazi kubwa katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Watanzania wenye asili ya India wanaoishi nchini Tanzania na serikali ya Tanzania, hali iliyosaidia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Shamim Khan amemshukuru Rais Kovind kwa kumtunuku tuzo hiyo ambayo ni heshima kubwa kwake.

Pia ameipongeza serikali ya India kwa kuendelea kudumisha ushirikiano wa kidugu na wa muda mrefu uliopo baina yake na  Tanzania na amemuomba Rais Kovind kuendelea kusaidia juhudi za serikali iliyo chini ya Rais John Magufuli katika kuwaletea maendeleo watanzania.Tuzo hiyo ya juu ya heshima hutolewa na Rais wa India kwa raia wenye asili ya nchi hiyo ambao wamekua wakitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi baina ya nchi wanazoishi na India.