Serikali yachunguza wanafunzi kufundishwa uovu

0
270

Serikali imetuma timu maalum kwenda mkoani Kilimanjaro kuchunguza tuhuma kuhusu wanafunzi kufundishwa vitendo vilivyo kinyume na maadili katika baadhi ya shule mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa elimu nchini, Mwanasheria wa wizara na Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora.

“Tumeshtushwa sana na jambo hilo, tumelichukua suala hili kwa umuhimu mkubwa tumeongea na mkuu wa mkoa na kama kuna jinai yeyote basi hatua za kisheria zichukuliwa mara moja”. amesema Waziri Mkenda

Amesema timu hiyo imeishaanza uchunguzi katika shule zilizotajwa na hatua za haraka zitachukuliwa kwa wahusika wote watakaobainika kuhusika.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa wizara ya Elimu itatoa namba maalum ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za vitendo hivyo viovu vinavyochafua taswira ya elimu, kuondoa imani ya wazazi kwa shule na inaharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.