SADC yazindua Kanzidata ya dawa

0
180

Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) imezindua Kanzidata maalumu kwa ajili ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa za dawa na vifaa tiba kutoka kwa wazalishaji na wazabuni mbalimbali duniani, ambapo mfumo huo utarahisisha upatikanaji na ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa nchi wanachama.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam na kushudiwa na maafisa kutoka Bohari za Dawa za nchi za SADC pamoja na viongozi mbalimbali wa sekta ya afya wa Jumuiya hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema mfumo huo utaziwezesha nchi wanachama wa SADC kupata taarifa za kina juu ya dawa na vifaa tiba kama vile sehemu zinapopatikana ama kutengezewa, pamoja na bei.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Tukai Mavere amesema Kanzidata hiyo itatumika kutunza taarifa za bidhaa za afya, nchi inakotoka, ubora wake, gharama yake na itasaidia kujua nchi tofauti zinapataje bidhaa zake na bei.