Rais Gotabaya Rajapaksa wa Sri Lanka ameripotiwa kuikimbia nchi hiyo kwa kutumia ndege ya kijeshi akiwa na mke wake, wakati huu ambapo bado maandamano makubwa yakiendelea nchini humo.
Rajapaksa mwenye umri wa miaka 73 kabla ya kukimbia nchini humo alikua amejificha mahali kusikojulikana, baada ya umati wa raia wa nchi hiyo kuvamia makazi yake Jumamosi iliyopita.
Wakati hayo yakiendelea, Waziri Mkuu wa Sri Lanka, Wickremesinghe ameteuliwa kuwa Rais wa muda wa Taifa hilo na tayari ametangaza hali ya hatari nchini humo.
Rajapaksa aliahidi kujiuzulu rasmi wadhifa wa Urais hii leo kufuatia maandamano makubwa ambapo waandamanaji wanapinga kupanda kwa gharama za maisha pamoja na kukosekana kwa nishati ya mafuta.
Naye Spika wa Bunge la Sri Lanka amekaririwa akisema kuwa,
Rais Rajapaksa atafanya taratibu za kuwasilisha barua rasmi ya kujiuzulu hii leo.
Amesisitiza kuwa kwa sasa Rais Rajapaksa yupo nje ya Sri Lanka na kwamba amewasiliana naye kwa njia ya simu na kumueleza kuwa atajiuzulu hii leo kama alivyoahidi siku ya Jumamosi.
Mpaka sasa haijafahamika kiongozi huyo emekimbilia nchi gani, lakini kuna tetesi kuwa huenda amekimbilia Marekani kwa kuwa kiongozi mwingine wa nchi hiyo ambaye ni Waziri wa zamani wa Fedha Basil Rajapaksa ameelekea katika nchi hiyo.