Rais Senegal akubaliana na mahakama uchaguzi kufanyika

0
260

Rais wa Senegal anasema uchaguzi uliocheleweshwa wa kuchagua mrithi wake utafanyika “haraka iwezekanavyo”. Hii ni baada ya mahakama ya juu kusema kwamba kucheleweshwa kwa uchaguzi huo ni kinyume cha katiba.

Rais Macky Sall amehudumu kwa mihula miwili na tayari amesema hatogombea tena kiti hicho. Hata hivyo, alitaka uchaguzi huo usogezwe hadi Desemba ili kuupa upinzani muda mzuri zaidi wa kujipanga.

Lakini wakosoaji wake walidai ni ‘janja’ yake ya kutaka kuendelea kubaki Ikulu.

Juzi Alhamisi, Mahakama ya Katiba ilibatilisha agizo la Rais Sall la kusogeza mbele uchaguzi huo.

Pia ilibatilisha muswada uliopitishwa na Bunge ukiunga mkono agizo la rais.

Hatua hiyo imeelezwa na baadhi ya wachambuzi kwamba itasaidia kwa kiasi fulani kurejesha sifa ya Senegal kama ngome ya demokrasia Afrika Magharibi.

Tangu alipotangaza kutaka kuchelewesha uchaguzi wiki mbili zilizopita, saa chache kabla ya kampeni kuanza, Rais Sall amekuwa kwenye shinikizo kubwa la kumtaka atengue uamuzi wake.