Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda yanaonesha Rais Yoweri Museveni anaongoza.
Rais Museveni anaongoza kwa kupata asilimia 65.02 ya kura zote zilizokwishahesabiwa huku mpinzani wake wa karibu
Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine akipata asilimia 27.39 ya kura hizo.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda, matokeo hayo ni kutoka katika vituo 8,310 vya kupigia kura kati ya vituo vyote 34, 684.
Katika taarifa yake, Serikali ya Uganda imeeleza kuwa uchaguzi wa Rais pamoja na Wabunge uliofanyika hapo jana ulikuwa huru na ulifanyika katika mazingira ya amani.