Rais Kenyatta atoa rambirambi ya shilingi Milioni 125

0
1923

Rais Dkt. John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kenya hapa nchini Dkt. Dan Kazungu na kupokea hundi ya shilingi Milioni 125 kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ikiwa ni rambirambi ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba 2018 katika ziwa Victoria.

Akizungumza baada ya kukabidhi rambirambi hiyo kwa Rais Magufuli, Balozi wa Kenya nchini amesema Wananchi wa Kenya wanaungana na Watanzania katika majonzi ya kuwapoteza watu 228 na wengine kujeruhiwa.

Kwa upande wake Rais Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Kenyatta na wananchi wa Kenya kwa kuguswa na ajali hiyo na ameahidi kuwa fedha hizo zitaelekezwa kuwasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya.

“Mwambie Mhe. Rais kuwa nashukuru sana, tulipanga fedha tulizopata tujenge wodi za wagonjwa lakini sasa tumeamua tujenge hospitali kubwa yenye hadhi ya Wilaya, na kwa mchango huu tunaweza kuamua wodi moja tukaiita Wodi ya Kenyatta” amesisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika  – SADC Dkt. Stergomena Tax.

Dkt. Stergomena Tax amesema amekutana na Rais Magufuli kumpa taarifa rasmi kuwa Mkutano wa 38 wa SADC uliofanyika tarehe 17 – 18 Agosti mwaka huu mjini Windhoek Namibia umemteua Rais Magufuli kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 2018 hadi Agosti 2019, na kwa maana hiyo Rais Magufuli ndiye atakuwa Mwenyekiti ajaye wa SADC kwa kipindi cha mwaka 2019/2020.

Kwa upande wake Rais Dkt. Magufuli amempongeza Dkt. Tax kwa kuteuliwa kwa mara ya pili kuwa Katibu Mtendaji wa SADC na pia amempongeza kwa kazi nzuri anazofanya katika Jumuiya hiyo.

Rais Magufuli amesema amepokea kwa heshima kubwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa SADC na kwamba yupo tayari kushirikiana na viongozi wenzake wa Jumuiya hiyo katika kutekeleza jukumu hilo.

“Nimepokea kwa heshima kubwa na nipo tayari kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na wenzangu” amesema Rais Magufuli.