Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis amelaani unyonyaji wa rasilimali unaofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kusababisha ufukara na migogoro katika Jamhuri hiyo.
Baba Mtakatifu Francis ametoa kauli hiyo mara baada ya kuwasili DRC kwa ziara ya siku tatu.
Amesema kitendo cha unyonyaji wa rasilimali hizo yakiwemo madini, hakipaswi kufumbiwa macho kwa kuwa kinaendeleza tabia za kikoloni ambazo zimekuwa zikihatarisha maendeleo ya Taifa hilo na raia wake.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema mataifa ya kigeni yanayotajwa kuhusika katika kusababisha migogoro inayoendelea katika baadhi ya maeneo huko DRC yanapaswa kuacha jambo hilo mara moja na kutazama namna bora ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo kunufaika na rasilimali zao.
Kwa upande wake Rais Felix Tshisekedi wa DRC amesema, migogoro inayoendelea nchini humo inasababishwa na makundi ya watu wenye silaha ambayo amedai yamekuwa yakisaidiwa na baadhi ya mataifa jirani na nchi hiyo.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani pia ameongoza misa maalumu iliyofanyika katika jiji la Kinshasa ambapo baadhi ya wakazi wa jiji hilo wamesema ujio wa kiongozi huyo ni neema kwa Taifa hilo kwa kuwa una lengo la kuendeleza amani, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wa DRC.
Ziara hiyo inafanyika ikiwa ni baada ya kupita takribani miaka 37 ambapo kwa mara ya mwisho nchi hiyo ilitembelewa na aliyekuwa kiongozi wa kanisa hilo marehemu Baba Mtakatifu John Paul wa Pili mwaka 1985.