Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Baba Mtakatifu Francis amewataka Maaskofu wa Kanisa hilo duniani kote kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya udhalilishaji badala ya kutoa kauli za kulaani tu vitendo hivyo.
Baba Mtakatifu Francis ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa siku nne wa viongozi wa Kanisa Katoliki unaofanyika kwenye Makao Makuu ya Kanisa hilo mjini Vatican.
Wakati wa mkutano huo, viongozi hao wa Kanisa Katoliki wanajadili kashfa ya vitendo vya udhalilishaji hasa kwa watoto.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani amewaeleza viongozi hao kuwa wakati umefika wa kuvigeuza vitendo hivyo vya udhalilishaji kuwa fursa ya uhamasishaji, utakasaji na kutibu majeraha makubwa yaliyosababishwa na vitendo hivyo.
Ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo kwa lawama kutoka kwa baadhi ya watu kuwa uongozi wa juu wa Kanisa Katoliki haujafanya jitihada za kutosha katika kukabiliana na vitendo hivyo vya udhalishaji.