Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis anatarajiwa kuwaongoza mamilioni ya waumini wa kanisa hilo katika ibada ya mazishi ya Papa Mstaafu Benedict XVI.
Kwa siku tatu mfululizo waumini wa Kanisa Katoliki wamepata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedict XVI mjini Vatican.
Kiongozi huyo wa kidini ambaye ni raia wa Ujerumani aliyefariki Jumamosi akiwa na umri wa miaka 95, aliliongoza Kanisa Katoliki kwa muda wa miaka nane kabla ya kuwa Papa wa kwanza katika kipindi cha karne sita kujiuzulu mnamo mwaka 2013.
Misa ya mazishi ya Papa Benedict itafanyika katika uwanja mkuu wa Mtakatifu Petro, kabla ya kuzikwa kwenye makaburi yaliyoko katika Kanisa la Mtakatifu Petro.
Papa Benedict alifariki katika nyumba ya watawa ya Mater Ecclesiae ndani ya bustani ya Vatican, ambayo yalikuwa makazi yake kwa muongo mmoja uliopita.