Kiongozi Mstaafu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa 16 amepinga pendekezo la mrithi wake, Papa Francis kuwaruhusu wanaume waliooa kutawazwa kuwa Makasisi katika eneo la Amazon.
Papa Benedict amesema hayo katika kitabu alichoandika kwa kushirikiana na Kadinali Robert Sarah kutoka nchini Guinea (From the Depths of Our Hearts: Priesthood, Celibacy and the Crisis of the Catholic Church) ambapo ameeleza kuwa utaratibu wa Makasisi kutokuoa umekuwapo kwa karne nyingi na huwasaidia Makasisi kuangazia zaidi kwenye majukumu yao.
Kiongozi huyo ambaye alistaafu mwaka 2013 amesema kuwa endapo pendekezo hilo likipitishwa itakuwa ni vigumu kwa Makasisi hao kutumiza majukumu yao ya kikanisa na ndoa kwa wakati mmoja.
Kitendo cha kiongozi huyo mstaafu kuzungumzia tukio hilo si cha kawaida kwani imezoeleka kiongozi mstaafu kutokumuingilia kiongozi aliyepo madarakani, lakini yeye amesema kwamba hakuweza kujizuia.
Pendekezo la kuwaruhusu wanaume waliooa kuwa Makasisi katika eneo Amazon limetokana na upungufu wa Makasisi ambapo kuna wakati mwezi mmoja hupita bila waumini kufanya ibada kutokana na kukosa kiongozi.