OUT kununua majengo Kinondoni

0
515

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiagiza wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukamilisha malipo ya majengo yanayotakiwa kununuliwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyopo eneo la Biafra, Kinondoni mkoani Dar es salaam.

Akizungumza alipotembelea makao makuu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyopo Kinondoni, Dar es salaam, Makamu wa Rais amesema hatua hiyo itakiwezesha chuo hicho kuwa na miundombinu ya kutosha.

Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya chuo hicho ili kiweze kutoa elimu bora na hasa inayolenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri, kushindana katika soko la ajira, kuwa wabunifu na kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi.

Aidha Dkt. Mpango ametoa wito kwa watafiti kujielekeza zaidi katika vipaumbele vya Taifa, ili kutatua changamoto mbalimbali.

Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuendeleza jitihada za vijana walioanzisha ubunifu unaotatua changamoto ikiwemo wale wanaotumia taka katika hatua za kutengeneza chakula cha mifugo na Samaki, wanaotengeza nishati mbadala pamoja na bidhaa za lishe zinazovutia watoto nchini.