ODINGA AYAKATAA MATOKEO YA UCHAGUZI KENYA

Uchaguzi Mkuu Kenya

0
208

Mgombea Urais wa Kenya kupitia tiketi ya Azimio la Umoja kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, Raila Odinga ameyakataa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa, akisisitiza kuwa hawatakubali kuona Mwenyekiti wa Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Wafula Chebukati anapindua maamuzi ya wakenya.

“Hatutakubali, narudia haya hatutakubali mtu mmoja ajaribu kuleta vurugu katika taifa letu, Wakenya hawatakubali, hatutakubali tutazidi kutetea katiba yetu kama Wakenya ili Kenya izidi kusonga mbele,” amesema Odinga.

Aidha, Odinga ameendelea kuwapongeza wafuasi wake kwa kuendelea kudumisha utulivu na amani iliyopo na kuendelea kuwasisitiza kuendelea kuwa watulivu wakati wao wakiendelea na taratibu zote za kuyakataa matokeo hayo kisheria.

Odinga amejitokeza leo baada ya tume kutangaza matokeo uchaguzi na kumtaja William Ruto kama mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika Agosti 9 mwaka huu.

Jana jioni Chebukati alitangaza kuwa Ruto ameshinda uchaguzi huo mkuu kwa asilimia 50.49 huku Raila Odinga akipata asilimia 48.85.