Watu wanane wakiwemo maofisa wa polisi wamelazwa hospitalini baada ya kutokea tukio la kutatanisha katika makao makuu ya huduma za usalama nchini Sweden.
Takriban watu 500 wameondolewa haraka kwenye jengo hilo baada ya wafanyakazi kuripoti kuvuta harufu isiyo ya kawaida.
Taarifa za awali zilionesha kwamba harufu hiyo inatokana na kuvuja kwa gesi, lakini vyombo vya usalama vimesema hakuna gesi iliyogunduliwa kuvuja ndani au nje ya jengo hilo.
Polisi wameanza uchunguzi wa awali ili kubaini chanzo cha harufu hiyo ya ajabu.
Mapema, vyombo vya habari vya ndani vilidai kugundua kuwepo kwa phosgene kwenye paa la jengo hilo, na kwamba ndio inaweza kuwa chanzo cha harufu hiyo, lakini mamlaka hazijathibitisha madai haya.
Phosgene hutumiwa kutengeneza plastiki na dawa za kuulia wadudu, na iliwahi kuhusika na vifo vingi vya kemikali wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.