‘Nabii’ hatiani kwa kudai anatibu Ukimwi

0
983

Mahakama nchini Zimbabwe imemtia hatiani mchungaji mmoja kwa makosa ya kughushi na imemtoza faini ya Dola 700 za Kimarekani kwa kudanganya kwamba ana dawa ya mitishamba inayoponya Ukimwi.

Awali Nabii huyo Walter Magaya alikiri kosa la kukiuka sheria ya udhibiti wa dawa kwa kuuza dawa ambayo haijathibitishwa na mamlaka zinazohusika.

Alikamatwa na polisi mwezi Novemba mwaka 2018 ambapo pia alipatikana na kidhibiti cha dawa alichokuwa akidai kwamba inatibu watu wenye virusi vinavyosababisha Ukimwi na Ukimwi.

Magaya mwenye umri wa miaka 35, mwezi Oktoba mwaka 2018 alisema kuwa dawa yake inayoitwa Aguma ina nguvu za kimiujiza za kutokomeza virusi vinavyosababisha Ukimwi ndani ya siku 14 na kwamba dawa hiyo haina madhara yoyote kwa watumiaji.

Ndipo polisi nchini Zimbabwe walipovamia ofisini kwake na kumfanyia upekuzi, kwa tuhuma za uhalifu.

Kabla ya kupekuliwa alijaribu kuharibu baadhi ya vidhibiti kwa kuvitumbukiza chooni na kuchoma moto baadhi ya maboksi yenye dawa hizo, ambapo hata hivyo polisi walizipata zikiwa zimeungua nusu.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, hadi mwaka 2016 watu milioni 1.3 walikuwa wakiishi na virusi vinavyosababisha Ukimwi nchini Zimbabwe.