Peter Anthony Morgan, mwimbaji kiongozi wa bendi maarufu ya reggae ya Morgan Heritage aliyoianzisha akiwa na ndugu zake wanne, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 46, familia yake imesema.
Familia imewashukuru watu kwa upendo na msaada wao. Hata hivyo, taarifa ya familia iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii haikueleza sababu za kifo cha mwanamuziki huyo kilichotekea jana Jumapili.
Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness amendika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba “moyo wake ni mzito” juu ya habari hiyo. Amekiita kifo cha Morgan “hasara kubwa” kwa Jamaica na muziki wa reggae duniani.
Morgan, anayejulikana kama “Peetah,” ni mtoto wa mwimbaji mashuhuri wa reggae kutoka Jamaica, Denroy Morgan.
Yeye na kaka zake waliunda Morgan Heritage mnamo 1994, na albamu yao ya “Strictly Roots” ilishinda tuzo ya Grammy ya albamu bora ya muziki wa reggae mwaka 2016.