Mwanamke Nigeria ajifungulia kituo cha basi

0
210

Mwanamke mmoja, amejifungua mtoto akiwa katika kituo cha mabasi katika Jiji la Lagos, Nigeria na kushangiliwa na umati wa watu waliokuwa wamekusanyika karibu na eneo hilo.

Mwanamke huyo ambaye jina lake halikutajwa alikuwa akisubiri kupanda basi kwenye Kituo cha Mabasi cha Onipanu wakati alipopata uchungu wa kujifungua ghafla, maofisa wa huduma za dharura wameiambia BBC.

Wafanyabiashara wa kike katika soko lililopo eneo hilo ndio waliogeuka wakunga, wakambeba hadi mahali penye utulivu na kumsaidia kujifungua mtoto wa kiume.

Baada ya kujifungua salama, mama na mtoto wakapelekwa hospitalini, kwa mujibu Shirika la Usimamizi wa Dharura la Jimbo la Lagos (Lamesa).

Habari za mwanamke huyo zimeteka mitandao ya kijamii Nigeria, baadhi wakipendekeza majina mbalimbali kwa ajili ya mtoto huyo.