Mvumbuzi wa kanda za kaseti afariki akiwa na miaka 94

0
299

Mvumbuzi wa kanda za kaseti aliyepata sifa na kutambulika kwa teknolojia hiyo ambayo ilitumika kuhifadhi muziki, Lou Ottens amefariki dunia.

Ottens amefariki dunia nyumbani kwake katika mji wa Duizel nchini Uholanzi akiwa na umri wa miaka 94.

Inakisiwa kuwa, zaidi ya kanda za kaseti bilioni 100 zimeshauzwa duniani tangu teknolojia hiyo ianze kutumika miaka ya 1960, huku ubunifu wa Ottens ukielezwa kufanikiwa kubadilisha kabisa namna watu walivyosikiliza muziki.

Kanda za kaseti hazifanyi vizuri sokoni katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ujio wa teknolojia mpya za Compact Disk (CD), ambayo na yenyewe iko njiani kutoweka kutokana na ujio wa teknolojia ya flashi.

Ottens, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Philips mwaka 1960 pamoja na timu yake, walitengeneza kwa mara ya kwanza mikanda ya kaseti ambapo mwaka 1963 kanda hizo zilitambulishwa katika maonesho ya redio jijini Berlin na hatimaye kufanya vizuri duniani.

Hata hivyo, Ottens aliingia makubaliano na kampuni za Philips na Sony ambapo kaseti ilipata hatimiliki, na baadaye baadhi ya kampuni za Kijapani kuanza kuzalisha kwa idadi kubwa.

Kwa mujibu wa kampuni za muziki nchini Uingereza, mauzo ya kaseti yalipanda kwa asilimia 103 mwaka 2020 ikilinganishwa na miaka ya nyuma, wakati nchini Marekani kwa mujibu wa kampuni ya muziki ya Nielsen mauzo ya kanda za kaseti yaliongezeka kwa asilimia 23 mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017.